Bawasiri na tiba zake
Bawasiri ni ugonjwa katika njia ya haja kubwa, hujitokeza kama uvimbe au kijinyama ambacho huweza kuonekana hadi nje. Kwa kiingereza hujuliakana kama haemorrhoids au piles.
Bawasiri inaweza kupelekea upungufu wa damu mwilini. Bawasiri inaweza kutibika ama kwa upasuaji ama kwa matumizi ya dawa mbadala kwa kipindi kirefu wiki hata 6 au hata zaidi kutegemea ilikuwa imejijenga kiasi gani.
Bawasiri husababishwa na nini
Hakuna sababu ya moja kwa moja inayojulikana kisayansi kwamba ndiyo husababisha bawasiri, bali mambo yafuatayo yanaweza kupelekea wewe kupatwa na ugonjwa huu:
- Kufunga choo au kupata choo kigumu kwa muda mrefu
- Ujauzito – wakati wa ujauzito watu wengine wanaweza kupatwa na bawasiri sababu ya msukumo wa mtoto karibu na sehemu ya kutolea haja kubwa
- Kushiriki mapenzi kinyume na maumbile
- Uzee – kadri miaka inavyosogea ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kupatwa na ugonjwa huu kwa baadhi ya watu
- Sababu za kurithi – baadhi ya watu wanaweza kurithi udhaifu wa ukuta huo wa njia haja kubwa ingawa ni asilimia ndogo sana.
- Kuharisha sana kwa muda mrefu
- Kutumia vyoo vya kukaa
- Kunyanyua vyuma vizito
- Mfadhaiko/stress
- Uzito na unene kupita kiasi nk
Dalili za bawasiri
- Maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa
- Damu kunuka kinyesi wakati wa kujisaidia
- Muwasho sehemu ya tundu la haja kubwa
- Uvimbe au kinyama kujitokeza sehemu ya tundu la haja kubwa
- Haja kubwa yaweza kujitokea tu muda wowote
Matibabu ya bawasiri:
Kutegemea na umri wako na namna ugonjwa ulivyojijenga na kudumu, unaweza kuhitaji dawa moja au mbili au hata tatu kwa pamoja kati ya hizi zifuatazo. Kumbuka kumshirikisha daktari wako kabla ya kuamua kuzitumia hizi dawa.
Bawasiri na tiba zake
1. Habbat-Sawdaa
Chukua kijiko kikubwa kimoja cha unga wa Habbat-Sawdaa ukoroge ndani ya glasi moja ya maji na unywe yote. Fanya hivi kutwa mara mbili kwa wiki mbili mpaka tatu hivi.
2. Habbat-Sawdaa na Asali
Changanya gm 500 za unga wa Habbat-Sawdaa na nusu lita ya asali. Lamba kijiko kimoja kikubwa cha chakula kila baada ya masaa manne. Ukimaliza kulamba kunywa glasi moja ya maji ya kunywa ya joto la kawaida.
3. Aloe Vera Fresh
Chukua kipande cha jani la mmea wa Aloe vera fresh (mshubiri) na kikate ukimenye kidogo ukitumia kidole kupata kama utomvu hivi au maji maji yake na upake sehemu ya utupu wako wa nyuma baada ya kuoga kutwa mara tatu. Jipake nyingi tu na uiache hivyo masaa kadhaa au mpaka utakpaoenda kuoga tena.
Tengeneza pia juisi freshi ya mmea huu na uchanganye nusu glasi dawa hii na nusu glasi nyingine ya juisi yoyote ya matunda uliyotengeneza nyumbani ili kupata glasi moja iliyojaa na unywe glasi 1 kutwa mara mbili kwa wiki 3 hadi 4. Juisi freshi ya aloe vera ni nzuri kwa kuongeza kinga ya mwili na kutoa taka zote za ndani ya mwili.
4. Juisi ya limau (lemonade)
Chukua juisi ya limau na upake sehemu iliyoathirika. Juisi ya limau sifa yake kuu hapa ni kuondoa sumu na kuongeza kinga ya mwili kwakuwa ina vitamin C kwa wingi. Pia unywe glasi moja ya juisi hii kutwa mara kwa wiki 3 hadi mwezi mmoja.
Lemonade inaandaliwa kwa kutumia limau, maji, asali na mdalasini ya unga kidogo, nayo inaandaliwa hivi:
*Chukua asali mbichi nusu Lita
*Chukua limau kubwa 12 au zaidi, zikate katikati kila moja. Zikamuwe moja baada ya nyingine kupata maji maji ya limau mpaka umepata ujazo wa nusu lita.
*Kwenye sufuria nyingine kubwa changanya mdalasini ya unga vijiko vikubwa 10 na maji lita 2 na nusu na uchemshe kama chai kisha ipua na uchuje na usubiri ipowe iwe ya uvuguvugu kidogo.
*Sasa changanya pamoja asali nusu lita, juisi au maji maji ya limau nusu lita, maji ya uvuguvugu ya mdalasini lita 2 na nusu ongeza na ya maji ya kawaida lita 1 kupata lita 5, chuja vizuri. Ihifadhi katika friji isiharibike.
Kunywa robo lita (ml 250) kutwa mara 2 kwa siku 30 hivi kwa mtu mzima na glasi ndogo moja kwa siku kwa mtoto wa miaka miwili mpaka kumi.
Unaweza pia kuongeza majani kidogo ya mnanaa (mint) na mbegu za shamari (fennel seeds) ili kuongezea radha na harufu nzuri.
Kunywa juisi hii kila unapokuwa umepata chakula cha mchana cha nguvu au cha jioni.
Unaweza pia kupakaa sehemu yenye bawasiri juisi hii ukitumia pamba kutwa mara 2. Unaweza kusikia maumivu zaidi lakini pole pole yataacha.
5. Siki ya tufaa
Chukua kipande cha pamba na ukichovyo ndani ya siki ya tufaa (apple cider vinegar) na ujipake kidogo kidogo eneo lenye uvimbe taratibu. Unaweza kusikia maumivu zaidi lakini jipe moyo taratibu yatapotea. Hakikisha unapata siki ya tufaa ile ya asili kabisa siyo ile iliyopita viwandani.
Pia kama una bawasiri ya ndani yaani ile isiyojitokeza nje na ukaiona kwa macho moja kwa moja unashauriwa kuchanganya kijiko kidogo kimoja cha siki ya tufaa ndani ya glasi ya maji na unywe yote kutwa mara 2. Hii husaidia pia kupunguza maumivu.
6. Mafuta ya nyonyo
Pakaa mafuta ya nyonyo mara mbili mpaka tatu kwa siku sehemu ya utupu wako wa nyuma kwa wiki tatu hadi nne hivi.
7. Mafuta ya lozi (Almond oil)
Yana uwezo wa kunyonya na kulainisha bawasiri hasa ya nje. Hivyo yanalainisha hicho kiuvimbe kinachojitokeza sehemu ya haja kubwa pia kuondoa maumivu kama utakuwa ukiyapaka kila siku.
Tumia pamba ukichovya ndani ya mafuta haya na upake sehemu yenye tatizo mara kadhaa kwa siku kwa wiki 3 hata mwezi mmoja.
8. Mafuta ya zeituni
Mafuta ya zeituni (Olive oil) ni moja ya dawa maarufu katika kutibu bawasiri. Mafuta haya yana viuavijasumu na huondoa pia maambukizi (infections). Yanaweza pia kusaidia kuongeza utanukani wa mishipa ya damu. Yanao uwezo pia wa kukausha kinyama cha bawasiri ya nje yakitumika kwa kupaka kwa kipindi kirefu.
Kunywa kijiko kidogo kimoja cha mafuta ya zeituni kila siku. Pia tumia pamba pakaa sehemu yenye tatizo nje na ndani kutwa mara 2 kila siku mpaka umepona.
9. Kipande cha barafu
Barafu inasaidia kubana mishipa na hivyo kuzuia uvimbe pia kuondoa maumivu kwa haraka.
Chukua kipande cha barafu na ukifunge ndani ya kitambaa kisafi na uweke moja kwa moja sehemu yenye tatizo kwa dakika 10 hivi. Fanya zoezi hili mara kadhaa katika siku. Zoezi hili linaondoa maumivu ya bawasiri na dalili zake.
10. Mafuta ya nazi
Mafuta ya nazi ni moja ya dawa nzuri sana kwa kutibu bawasiri. Mafuta ya nazi ni dawa nzuri dhidi ya bakteria, virusi na vijidudu nyemelezi sifa ambazo zinayafanya kuwa bora kwa kutibu bawasiri.
Mhimu yawe ni mafuta ya asili kwa asilimia 100 bila kuongezwa kingine chochote ndani yake na hayajapita kiwandani.
Safisha vizuri sehemu yenye tatizo na ukaushe na kitambaa, chukua pamba chovya mafuta ya nazi na upake sehemu yenye tatizo nje na ndani kutwa mara 3 kwa majuma kadhaa.
11. Maziwa ya mbuzi
Kama unasumbuliwa na bawasiri ya ndani na inakusababishia kuwa unapata choo chenye damu unatakiwa ujaribu maziwa ya mbuzi. Hii ni moja ya dawa rahisi zaidi za kutibu bawasiri ya ndani.
Chukua nusu kijiko kidogo kimoja cha unga wa mharadali (mustard) uchanganye na vijiko vikubwa 10 vya maziwa ya mbuzi na unywe kabla ya chakula cha asubuhi kila siku.
12. Binzari
Binzari au manjano inao uwezo wa kuzuia na kutibu magonjwa. Hivyo inaweza kutumika pia kutibu sehemu iliyoathirika na bawasiri.
Namna ya kutumia: chukua binzari ya unga kijiko kidogo kimoja changanya na mafuta ya mharadali na maji maji ya kitunguu maji na upate uji mzito (paste). Pakaa moja kwa moja huu mchanganyiko sehemu yako ya utupu wa nyuma na uache huko kwa dakika kadhaa.
Hii inasaidia kutibu majeraha na kupunguza uvimbe mara moja. Tumia kwa majuma kadhaa.
13. Unga wa Mbegu za maembe
Kutumia mbegu kubwa za maembe ni namna nyingine rahisi ya kutibu bawasiri hasa ya ndani inayotoa damu.
Tumia kama ifuatavyo:
Chukua mbegu za maembe (kokwa) toka katika maembe yaliyoiva, zianike juani kwa siku kadhaa na zikikauka kabisa zitwange au peleka mashineni upate unga wake na uuhifadhi unga ndani ya chupa isiyopitisha hewa.
Kisha changanya gramu 2 za unga huu na kiasi kidogo cha asali na ulambe yote. Fanya hivi kutwa mara 2 kwa majuma kadhaa.
Kwa faida ya ziada ni kuwa Unga huu wa mbegu za maembe hutumika pia kukaza uke uliolegea au ulioongezeka sana ukuwa.
14. Baking Soda
Tafiti nyingi zinasema baking soda ina faida kubwa pia katika kutibu bawasiri. Unatakiwa kuchanganya unga huu na maji kidogo kasha upake moja kwa moja sehemu yenye tatizo.
Hii inasaidia kupunguza maumivu na kuondoa dalili za bawasiri. Baking soda ni ile wamama wanaitumia kupika maandazi hata mikate wakati mwingine inapatikana kwenye maduka ya kawaida hata Mangi hapo nje anayo.
Kwanini watu wengi hawaponi bawasiri? :
Dawa peke yake haziwezi kukuletea maajabu yoyote, unaweza kupona lakini kama hutabadili vifuatavyo ugonjwa utaendelea kujirudia kwako na pengine hata kupona itakuwa shida. Bawasiri huwa haiponi haraka, walau dozi yake isiwe chini ya mwezi mmoja na ukizingatia yafuatayo kwa kipindi kirefu basi kupona ni lazima.
WaTanzania wengi wanaugua bawasiri kutokana na sababu kuu mbili, moja wanakula ugali wa sembe badala ya ugali wa dona, pili hawanywi maji ya kutosha kila siku na wengine hawanywi maji mpaka wasikie kiu.
Ili upone bawasiri moja kwa moja kwa urahisi zaidi zingatia yafuatayo kila siku:
- Kula vyakula vingi vyenye nyuzinyuzi (fiber) kila siku
- Kunywa maji mengi kila siku ili kusafisha mwili na kuepuka kufunga choo
- Kula sana mboga majani na matunda
- Kula vyakula ambavyo havijakobolewa
- Epuka mapenzi kinyume na maumbile
- Fanya mazoezi ya kuchuchumaa na kukaa mara 1 kila siku (squatting)
- Usitumie choo cha kukaa
- Usikae kwenye kiti masaa mengi
No comments:
Post a Comment